
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimetaka kukomeshwa mara moja vitendo vya unyanyasaji wa wananchi katika jimbo la Ushetu, na wilaya nzima ya Kahama.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa (CCM), Shaka Hamdu Shaka, ametoa agizo hilo juzi Jumamosi wakati wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Ushetu, wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga.
Shaka amesema CCM haitaki kusikia aina yoyote ya unyanyasaji dhidi ya wananchi, huku akitaka miongoni mwa manyanyaso hayo ni pamoja na ukamataji usio na staha hususan kwa wale wanaodaiwa kukutwa na mazao ya misitu ikiwamo mkaa.
“Nimeelezwa na wananchi kuwa moja ya changamoto hapa Ushetu ni maofisa wa TFS (Wakala wa Huduma za Misitu) kuwakamata wananchi katika namna ya manyanyaso ikiwamo kuwadhuru na kuwaharibia vifaa vyao kama baiskeli wanazozitumia kusafirisha mkaa.
“Jambo hili sio sawa, kama kuna tatizo, njia bora ya kukabiliana nalo ni kutumia namna sahihi za kisheria, siyo kuwashambulia, kuwaharibia vifaa na wakati mwingine kuwadhuru maungoni,” amesema.
Wakati huo huo Shaka amelitaka Jeshi la Polisi wilayani Kahama kukomesha tabia ya baadhi ya askari wake wanaodaiwa kuwabambika kesi wananchi kwa madai ya kukamatwa na bangi.
Shaka amesema wapo baadhi ya askari polisi wanaotumia kisingizio cha biashara ya bangi kuwakamata wananchi na kuwaweka mahabusu bila kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
Amesema kutokana na dosari hizo mbili, atazungumza na wahusika, akiwamo Waziri wa Maliasili na Utalii kwa upande wa tatizo linalohusiana na madai ya mazao ya misitu, pia atazungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro, ili hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika.
