
MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
Mtaalam wa virutubisho tiba, Abdallah Mandai, ameishauri jamii kujenga utaratibu wa kutumia viazi vyekundu (Bitruti), kunufaika na faida zake mwilini.
Amesema viazi hivyo vina madini ya nitrate kwa wingi ambayo yanasaidia kutanua na kulainisha mishipa ya damu, hivyo kupunguza uwezekano wa mtumiaji kukumbwa na shinikizo la damu na pia huimarisha kuta za ndani za mishipa ya damu.
Mandai ametoa rai hiyo leo Machi 20, 2023, jijini Dar es Salaam, katika utaratibu wake wa kutoa elimu kwa jamii kuhusu vyakula wanavyopaswa kula ili kuikinga au kuitibu miili yao.
“Unaweza kutumia viazi vyekundu kama juisi baada ya kusaga, unaweza kunywa glasi moja ya juisi ya viazi vyekundu kila siku peke yake au zaidi ya glasi moja kila siku kama ukiwa umechanganya na matunda mengine.

“Viazi hivi vyekundu vina madini ya potasiamu, chuma, vitamini A, B6 na C, asidi ya foliki, protini na wanga.
“Pamoja na kusaidia kupunguza shinikizo la damu, faida nyingine ya viazi vyekundu ni kuongeza damu mwilini na kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo na kuboresha mzunguko wa damu kwenye ubongo hasa kwa wazee, ” amesema Mtaalam Mandai.
Aidha, Mandai ametoa mwito kwa yeyote mwenye tatizo la kiafya aende katika kituo chake cha kutolea huduma za afya, Ukonga Mongo la Ndege, jijini Dar es Salaam ambapo wanamjali mgonjwa yeyote na wanatumia virutubisho tiba asili kukabiliana na matatizo mbalimbali ya kiafya.
